Genesis 44

Kikombe Cha Fedha Ndani Ya Gunia

1Kisha Yosefu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu kwenye mdomo wa gunia lake. 2 aKisha weka kikombe changu kile cha fedha kwenye mdomo wa gunia la yule mdogo wa wote pamoja na fedha zake ambazo angenunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yosefu alivyosema.

3 bKulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda zao. 4Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yosefu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja, utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya? 5 cJe, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu na pia hukitumia kwa kutabiri mambo yajayo? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”

6Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao. 7 dLakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako wasije wakafanya jambo kama hilo! 8 eHata hivyo tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye midomo ya magunia yetu. Hivyo kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani kwa bwana wako? 9 fIkiwa yeyote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”

10Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Yeyote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”

11Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua. 12Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini. 13 gKwa jambo hili, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda zao na kurudi mjini.

14 hYosefu alikuwa bado yuko nyumbani mwake wakati Yuda na kaka zake walipoingia, wote wakajitupa chini mbele yake. 15 iYosefu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kutabiri?”

16 jYuda akajibu, “Tutaweza kusema nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi wenyewe pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”

17Lakini Yosefu alisema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine, rudini kwa baba yenu kwa amani.”

18 kNdipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe. 19Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’ 20 lNasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’ 

21 m“Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’ 22Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’ 23 nLakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’ 24 oTuliporudi nyumbani kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.

25 p“Ndipo baba yetu aliposema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’ 26 qLakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutakapokwenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’

27 r“Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili. 28 sMmojawapo alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo. 29 tIkiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’

30 u“Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu, 31akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. 32Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sikumrudisha kwako nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’

33“Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake. 34Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”

Copyright information for SwhNEN